Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Madini la Taifa

*STAMICO YAKABIDHIWA LESENI YA KUCHIMBA NICKEL- NTAKA, NACHINGWEA LINDI*

Imewekwa: 23 July, 2025
*STAMICO YAKABIDHIWA LESENI YA KUCHIMBA NICKEL- NTAKA, NACHINGWEA LINDI*

8/7/2025  Nachingwea , Lindi

 

 *_Ni hatua kubwa ya kuendelea kuimarisha STAMICO_* 

 

 *_Waziri Mavunde ailekeze STAMICO  kuanza uchimbaji ndani ya Miezi 18_* 

 

 *_Wachimbaji wadogo  waliokuwa wakichimba maeneo ya Ntaka kupewa lesnii  na kurasimishwa*_ .

 

Waziri wa Madini Mhe. Anthony P. Mavunde katika kijiji cha Nditi amekabidhi kwa Shirika la Madini la Taifa ( *STAMICO* ) leseni ya Nickel iliyoko katika eneo la Ntaka iliyokuwa inamilikiwa na Serikali.

 

 Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo Mhe. Mavunde ameitaka *STAMICO* kuanza utekelezaji wa shughuli za uchimbaji mkubwa katika leseni hiyo ndani ya kipindi cha miezi 18. Aidha, kwa kutambua mchango wa wachimbaji wadogo kwenye pato la taifa, Mhe. Mavunde amemwelekeza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi kuhakikisha wachimbaji wadogo waliokuwa Ntaka wanagawiwa maeneo ya uchimbaji.

 

 Akipokea uamuzi wa Serikali wa kuipatia *STAMICO* leseni ya Nickel, Mkurugenzi Mtendaji wa *STAMICO* Dkt. Venance B. Mwasse amesema *STAMICO* inatoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake kupitia Waziri wa Madini wa kuipatia *STAMICO* leseni ya kuchimba nickel. Dkt. Mwasse aliongeza kuwa *STAMICO* inapokea uamuzi huu kwa mikono miwili na yeye pamoja na timu ya watumishi watatekeleza kazi hii ya uwekezaji kwa bidii na kuleta tija kwa wakati. Kwa wakazi wa kijiji cha Nditi. Dkt. Mwasse amewahakikishia kuwa uwekezaji wa *STAMICO* utazalisha ajira za kutosha, utaongeza mchango wa mgodi kwa jamii kwa kuchangia kikamilifu kwenye miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa madarasa, miundo mbinu ya maji na barabara.

 

 Naye  Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mh  Zainab Telack akiongea katika hafla hiyo amesema hana shaka na uwezo wa *STAMICO* katika kuiendeleza leseni waliyopewa. Akionyesha kuridhishwa na kazi za *STAMICO* , Mh. Telack amesema *STAMICO* imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya Mkoa wa Lindi  kwa kujenga kiwanda cha kusafisha chumvi katika Wilaya ya Kilwa. Vile vile kwa miaka mitatu mfululizo *STAMICO* imeshiriki katika maonyesho ya madini ya Mkoa wa Lindi na kutoa mafunzo kwa wazalishaji wa chumvi. Mh. Telack aliongeza kuwa Mkoa wa Lindi una madini ya aina nyingi yanayohitaji kufanyiwa   utafiti wa kijiolojia ili kasi ya uwekezaji iongezeke. 

 

Nae mbunge wa Jimbo la Nachingwea Mhe. Dkt. Amandus Chinguile akiongea katika hafla hiyo amesema, amefurahi kuona kuwa suala alilolipigania kwa jitihada kubwa na lililosubiriwa na wananchi kwa muda mrefu leo linatimia. Aidha Mhe. Mbunge ameitaka *STAMICO* kuharakisha uwekezaji ili Halmashauri na wananchi wa Nachingwea waweze kunufaika. 

 

Akihitimisha katika hafla hiyo, mwenyekiti wa LIREMA ndugu Mayunga alishukuru kwa ujio wa *STAMICO* na kuiomba kuwakumbuka wachimbaji wa Ntaka kwenye mgao wa mashine za uchorongaji zilizonunuliwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo. 

 

Hafla ya makabidhiano ilipambwa kwa shamrashamra za wasanii mbalimbali pamoja na wananchi wakazi wa Nditi.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo