Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

STAMICO KINARA WA MAGEUZI, MHE. RAIS AIMWAGIA PONGEZI, YAIBUKA NA TUZO YA RAIS KWA MARA YA PILI


● Yapongezwa utoaji wa gawio la bilioni 9 kwa Serikali 2018\19-2023\24

●Rais, Dkt.Samia aipongeza STAMICO kwa kukusanya bilioni 85 katika mwaka 2023/2024

● Yapata tuzo ya Ufanisi Katika Utendaji (Operational Excellence And Financial Performance )

*Arusha*

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amelipongeza Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa mageuzi makubwa ya kiutendaji yaliyopelekea Shirika kuendesha miradi yake kwa faida kubwa.

Dkt.Samia amesema hayo leo Agosti 28, 2024 wakati akihutubia katika Kikao Kazi cha Watendaji Wakuu na Wenyeviti wa Bodi wa Taasisi za Umma kinachoendelea mkoani Arusha.

Dkt. Samia amesema kuwa, STAMICO imefanya mageuzi makubwa yenye faida kwa Serikali ambapo katika Mwaka wa Fedha 2018\2019 STAMICO iliweza kukusanya shilingi bilioni 1 na baada ya Serikali kupitia Msajili wa Hazina kuliwezesha Shirika sasa linafanya mageuzi makubwa katika sekta ya madini nchini.

Rais Dkt.Samia ameeleza kuwa, mchango wa wachimbaji wadogo kwenye mnyororo mzima wa sekta ya madini umefikia asilimia 40 hii ni kutokana na usimamizi mzuri wa STAMICO.

Akielezea kuhusu gawio kwa Serikali , Dkt.Samia ameipongeza STAMICO kwa kutoa gawio la shilingi bilioni 9 kuanzia kipindi cha Mwaka wa Fedha 2018\19 hadi 2023\2024.

Nae , Msajili wa Hazina Tanzania Nehemia Mchechu amesema Sheria mpya inatungwa ili kusimamia Mashirika na Taasisi za umma katika kukuza ufanisi na uwajibikaji ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt. Samia Hassan.

Kwa upande , Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ,Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo amesema Rais Dkt.Samia amefungua nchi katika fursa za kiuchumi na kidiplomasia hivyo ameyataka mashirika ya umma kutumia fursa hiyo kuimarisha na kufungua uwekezaji ndani na nje ya nchi.

Sambamba na pongezi hizo, STAMICO imepewa tuzo ya Ufanisi Katika Utendaji (Operational Excellence And Financial Performance ) kutoka kwa Msajili wa Hazina inayotambua Mashirika ya Umma yanayojiendesha kibiashara kwa faida ambayo yameondokana na utegemezi kutoka Serikali kuu

STAMICO imepokea tuzo hii kutoka kwa Msajili wa Hazina kwa mara ya pili mfululizo tangu mwaka 2023 ambapo ilipata tuzo mbili ikiwemo Tuzo ya mashirika yaliyofanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji na yenye tija pamoja na tunzo ya mashirika ya umma ambayo yametoa Gawio kwenye mfuko wa Serikali 2023.