News
STAMICO YAPELEKA MKAA MBADALA WA RAFIKI BRIQUETTES HANDENI-TANGA
*MKUU WA WILAYA WAKILI ALBERT MSANDO AIPONGEZA STAMICO KWA KUSUKUMA AJENDA YA KITAIFA YA NISHATI SAFI*
Shirika la Madini la Taifa(STAMICO ) tarehe 16 Disemba,2024 imeshiriki Tamasha la wiki ya Marafiki wa Maendeleo Handeni (MMAHA) lenye lengo la kuhamasisha upimaji wa afya na kutoa matibabu kwa wananchi wa Handeni, pia utunzaji wa mazingira na matumizi sahihi ya Nishati Mbadala ya Rafiki Briquettes.
Akizindua Tamasha hilo Mkuu wa Wilaya ya Handeni Wakili Msomi Albert Msando amewasihi wananchi kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika Tamasha hilo litakalo ambatana na Matukio mbalimbali ikiwemo Upimaji wa afya kutoka Kwa Madaktari bingwa toka Hospital ya Taifa Muhimbili na JKCI , Elimu juu ya ajenda ya kitaifa ya Matumizi sahihi ya nishati safi na Salama ya Kupikia ya Rafiki Briquettes inayozalishwa na STAMICO, Semina kuwaweza kiuchumi Makundi maalum, na Mafunzo toka kwa Wataalam wa tiba za asili toka Wizara ya Afya.
Wakati wa hotuba yake ya Ufunguzi wa Tamasha hilo Mkuu wa Wilaya alitumia fursa hiyo kuishukuru Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kukubali wito na kushiriki kikamilifu kwa kuja kutoa elimu na hamasa ya utunzaji wa mazingira na matumizi sahihi ya Nishati Mbadala ya Rafiki Briquettes ambapo ni jitihada zakupongezwa katika Kusukuma ajenda ya Kitaifa ya Matumizi ya nishati safi ya Kupikia.
Nae Mwenyekiti wa Taasisi hiyo isiyo ya Kiserikali ya Marafiki wa Maendeleo Handeni (MMAHA) Bi Mariam Mwanilwa ameipongeza Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa STAMICO kwa kuona tija ya kuja na Nishati Mbadala ya Rafiki Briquettes itakayokwenda kutumiwa na watu wengi zaidi, na kuwasihi wanahandeni kuwa fursa imekuja waichangamkie wakawe mabalozi wazuri wakutunza mazingira asilia ya Handeni kwa kutumia Nishati Safi ya Rafiki Briquettes.
Kwa upande wa STAMICO, Afisa Masoko Mwandamizi Bilton Otto amewapongeza waandaaji wa Tamasha hilo na Kuwashukuru kwa Kuwaalika STAMICO kushiriki katika Kutoa elimu ya nishati safi na Salama ya Kupikia ya Rafiki Briquettes na kutumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wa Handeni kuunga mkono jitihada za Serikali na ajenda ya kutokomeza matumizi ya Nishati zisizo salama na badala yake watumie Rafiki Briquettes kama chanzo cha Nishati katika shughuli zao za kila siku,Pia alitumia fursa hiyo kuwaalika wananchi Kujitokeza kwa Wingi kuhudhuri Semina ya Nishati safi na Salama ya Kupikia ya Rafiki Briquettes itakayotolewa Siku tarehe 18 Disemba 2024 katika Ukumbi wa CCM Wilayani Handeni.
Awali Tamasha hilo lilitanguliwa na Matembezi ya Kilomita mbili toka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Handeni hadi Viwanja vya Handeni Square.
Tamasha ilo litahitimishwa rasmi tarehe 21 Disemba 2024.