News
STAMICO YAONGEZA MTAMBO WA UCHORONGAJI KUIMARISHA UFANISI KWA WATEJA
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeendelea kujiimarisha katika shughuli za Utafiti wa madini Nchini. Hii ni baada ya kununua Mtambo mwingine mpya wa kisasa wa Reverse Circulation (RC) kwa ajili ya shughuli za Uchorongaji miamba.
Mtambo huu (Rig) una uwezo wa kuronga hadi mita mia tatu (300) chini ya ardhi. Mbali na uchorongaji wa RC, mtambo pia una sifa ya uwezo wa kuchoronga staili nyingine za Rotary Air Blast (RAB) pamoja na Air Core (AC).
Ujio wa Mtambo huu mpya, umelifanya Shirika kuwa na jumla ya mitambo minne (4) ya kisasa ya Reverse Circulation (RC).
Hakika, mtambo huu ni matunda ya matokeo makubwa ambayo Shirika linaendelea kufanya katika kandarasi za Uchorongaji miamba unaolenga tafiti za madini kwa Wachimbaji Wadogo, Wakati na Wakubwa hapa nchini. Shirika linaendelea pia kutoa huduma katika tafiti nyinginezo kama Joto Ardhi na Mafuta.
Mtambo huu umewasili tarehe 9 February, 2025 katika mgodi wa ubia wa BUCKREEF na STAMICO uliopo katika kijiji cha Rwamgasa, Kata ya Katoro Mkoani Geita kwa ajili ya kusaidia shughuli za uchorongaji katika eneo la Uzalishaji (Pit) na utafiti maeneo ya jirani na mgodi.