Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

MWENYEKITI WA BODI YA STAMICO ATAJA FAIDA ZA USHIRIKI WA MAONESHO YA MADINI


Mwenyekiti Wa Bodi ya Wakurugenzi Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo amewataka wananchi pamoja na makampuni makubwa yanayohusika na masuala ya madini kuhudhuria maonesho ya 5 ya teknolojia ya Madini ili kuona mtambo wa kisasa wa uchorongaji wa STAMICO.


Amewataka wananchi kutembelea banda la STAMICO ili kujionea mitambo ya kisasa ya uchorongaji ambayo itawawezesha kujua na kupata taarifa sahihi za kiasi cha madini yaliyopo katika maeneo yao.


Akizungumza wakati anatembelea mabanda mbalimbali katika maonyesho hayo Mej. Jen. Isamuhyo amesema mtambo huo ni wa kwanza Tanzania kwani unafanya kazi kwa kutumia rimoti ni mzuri kiusalama na unarahisisha huduma.


Amesema mtambo huo wa kisasa wa uchorongaji na utafiti wa madini aina Reverse Circulation ( RC) ni bora kwani hata waendeshaji wake ni tofauti na mitambo mingine ambayo imekuwa ikitumia nguvu za binadamu.


Aidha Mwenyekiti huyo wa Bodi STAMICO amesema uchorongaji ndio njia pekee inayosaidia kupata taarifa na data sahihi za kiwango cha madini kilichopo katika maeneo mbalimbali hasa madini aina ya dhahabu.


‘STAMICO kwa sasa inakwenda kuzuri zaidi kwani tunatumia teknolojia ya kisasa katika mitambo mbalimbali tuliyonayo ambayo watu wengi hasa wachimbaji wadogo wanashughulika nayo’ ameongeza Mej. Jen. Isamuhyo


Ametoa pongezi kwa waandaaji wa maonesho na kusema, kupitia Maonyesho hayo wameweza kuonyesha vifaa ambavyo STAMICO wanavyo lakini pia kuwaelimisha wananchi juu ya masuala madini pamoja na teknolojia ya uchimbaji kwa ujumla.


Amesema maonesho haya yanatoa fursa kwa wadau kujifunza, kuunza vifaa vinavyohusika na madini na pia kutanua wigo wa biashara na uwekezaji.


Ametoa wito kwa wadau mbalimbali kutumia maonesho hayo kujifunza na kushauri kuwa ni vyema yakaendelea kufanyika kila mwaka na hata katika mikoa mingine ambayo ina madini kwani yatasaidia wananchi kutembelea na kujifunza kuhusu shughuli za madini zinazofanywa.