Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

State Mining Corporation

State Mining Corporation

News

Hati ya makubaliano na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)


STAMICO NA TANESCO KUSHIRIKIANA KUZALISHA UMEME KWA MAKAA YA MAWE YA KIWIRA

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limesaini hati ya makubaliano na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kutekeleza Mradi wa kufufua umeme wa Megawati 200 kwa kutumia Makaa ya Mawe yanayopatikana Kiwira mkoani Songwe.

Makubaliano haya yamefikiwa leo Agosti 10, 2021 baada ya kukamilika kwa zoezi la utiaji saini wa Hati ya Makubaliano uliofanyika ofisi za TANESCO Makao Makuu Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi na wataalamu kutoka katika Taasisi hizo mbili.

Akielezea umuhimu wa makubaliano hayo Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amesema utekelezaji wa mradi huu unaenda kuyaongezea thamani madini ya makaa ya mawe kwa kuwa kwa muda mrefu yamekuwa hayatumiki kimamilifu katika uzalishaji wa umeme kwa ajili ya kulisha kwenye gridi ya Taifa.

Dkt. Mwasse amesema, amefurahi kuona umefika wakati sasa Taasisi za Serikali zinashirikiana katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo na makubaliano haya ni mwanzo wa utekelezaji wa mradi huu ambao unaenda kuongeza ajira kwa watanzania na kuboresha uchumi wa wazawa wa maeneo hayo.

Ameongeza kwa kusema taasisi hizi mbili zinafanya kazi tofauti lakini zinategemeana katika kuliletea Taifa maendeleo. Hivyo mashirikiano hayo yataiwezesha STAMICO kuongezea thamani katika madini ya makaa ya mawe wakati huohuo TANESCO inapata Malighafi zitakazowawezesha kuzalisha umeme wa kutosha ili kukidhi mahitaji ya nchi na kuwezesha uwepo wa viwanda nchini.

Aidha ametumia nafasi hiyo kuushukuru uongozi wa TANESCO kwa kushirikiana bega kwa bega tangu STAMICO ilipoanza mchakato wa kuhuisha mradi huu unaolenga kuokoa rasilimali madini zilizopo katika mgodi ili ziweze kuwanufaisha watanzania

Akiongea kwa upande wa TANESCO Mkurugenzi Mtendaji Mhandisi Tito Mwinuka amesema makubaliano haya ni hatua ya awali inayotoa nafasi kwa kila Taasisi kufanya majukumu yake kwa mujibu wa makubaliano, ambapo hatua hii itafuatiwa na kufanyika kwa upembuzi yakinifu ili kuweza kubainisha mambo mbalimbali ikiwemo teknolojia na gharama halisi ya utekelezaji wa mradi huu.

Amebainisha majukumu ya kila Taasisi katika makubaliano hayo.